Wafanyakazi kuendelea kutozwa ada ya nyumba, hatima kujulikana Januari 26

Martin Mwanje
2 Min Read

Wafanyakazi nchini wataendelea kutozwa ada ya nyumba hadi mahakama ya rufaa itakapotoa uamuzi kuhusu utozwaji wa ada hiyo Januari 26, 2024. 

Ada hiyo ilitajwa na mahakama kuu kuwa kinyume cha katiba, hatua iliyoifanya serikali kupinga uamuzi huo katika mahakama ya rufaa.

Serikali inataka wafanyakazi kuendelea kutozwa ada hiyo hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa.

“Baada ya kusikiliza pande zote, maombi yote yamejumuishwa pamoja kwani yanatokana na hukumu sawa ya mahakama kuu iliyotolewa Novemba 28, 2023. Kesi nambari E577/2023 imetajwa kama faili kuu. Uamuzi kuhusiana na maombi yaliyojumuishwa utatolewa Januari 26, 2024,” walisema majaji wa mahakama ya rufaa Lydia Achode, John Mativo na Paul Gachoka katika agizo lao.

“Wakati huohuo, hali ilivyo kwa sasa kufikia leo itaendelea hadi uamuzi huo utakapotolewa.”

Serikali kupitia ada hiyo inakusudia kutekeleza mpango wa nyumba za gharama nafuu, mpango ambao inasema itahakikisha watu wenye kipato cha chini wanamiliki nyumba na kuishi katika makazi bora.

Hata hivyo, kesi iliyowasilishwa dhidi ya mpango huo mahakamani ni moja ya sababu ambazo zimemfanya Rais William Ruto kuinyoshea idara ya mahakama lawama, akisema inashirikiana na watu fulani kuhujumu utekelezaji wa mipango ya serikali.

Ameapa kuhakikisha hulka hiyo haikiti mizizi chini ya utawala wake, matamshi ambayo yamekosolewa vikali na taasisi mbalimbali na upinzani.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu Martha Koome amewataka majaji kusimama imara na kuhakikisha haki inadumishwa katika utendakazi wao.

 

 

 

Share This Article