Harambee Stars kukabana koo na Zimbabwe leo jijini Kampala

Dismas Otuke
1 Min Read

Timu ya taifa ya soka Harambee Stars itashuka katika uwanja wa Nelson Mandela mjini Kampala kupambana na Zimbabwe, katika mchuano wa kwanza wa kundi J kufuzu kwa fainali za AFCON mwaka 2025.

Pambano hilo litang’oa nanga saa kumi alasiri na kurushwa mubashara na runinga ya taifa KBC Channel 1.

Timu hizo zinakutana kwa mara ya tano ,Kenya ikishinda mechi tatu na kutoka sare mchuano mmoja.

Harambee Stars  iliwashinda The Warriors ya Zimbabwe mabao 2-0 katika mchuano wa kufuzu kwa kombe la  Dunia mwaka 2008, jijini Nairobi na kutoka sare tasa mjini Harare.

Kenya iliishinda Zimbabwe mabao 3-1 katika mchuano wa kirafiki mwezi Machi mwaka huu, na kisha kuibwaga tena mabao 2-0, katika mechi ya kuwania kombe la COSAFA mwezi Julai mwaka .

Vijana wa kocha Engin Firat baadaye watazuru Afrika Kusini kesho, kwa mechi ya pili dhidi ya The Brave Warriors ya Namibia Jumanne ijayo.

Mechi hizo zitakamilika mwezi Novemba huku  timu mbili bora zikifuzu kwa fainali za AFCON zitakazoandaliwa nchini Morocco kati ya Disemba mwaka ujao na Januari mwaka 2026.

Share This Article