Timu ya taifa ya soka ya kina dada Harambee Starlets imefuzu kwa raundi ya pili wa michuano ya kufuzu kwa fainali za kombe la bara Afrika.
Hii ni baada ya kuishinda Cameroon mabao manne kwa matatu kupitia penalti kwenye mkondo wa pili wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo uwanjani Nyayo jijini Nairobi.
Cameroon ilishinda mechi ya mkondo wa kwanza nyumbani kwa bao moja kwa bila huku Starlets waking’ang’ana na kushinda mechi ya leo kwa bao moja kwa bila.
Raundi ya kwanza kati ya timu hizo mbili ilikamilika kwa bao moja kwa moja baada ya mikondo miwili na kulazimisha uamuzi kupitia penalti.
Katika raundi ya pili, Novemba 2023, Starlets itachuana na Botswana ambayo ilifuzu kwa kuishinda Gabon alama 9 kwa moja.
Timu itakayoshinda katika raundi ya pili itafuzu moja kwa moja kwa fainali za kuwania kombe la bara Afrika kwa kina dada, mashindano ambayo yataandaliwa mwakani nchini Morocco.