Timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Kenya, Harambee Starlets, iliambulia kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Benin katika mchuano wa kirafiki uliosakatwa Jumatatu usiku katika
uwanjani Félix Houphouët-Boigny mjini Abidjan, Ivory Coast.
Nailatou Sadikou na Yolande Gnammi walipachika bao moja katika kila kipindi na kuwahakikishia Benin ushindi.
Kenya ilitumia pambano hilo kujiandaa kwa kipute cha bara Afrika (WAFCON) kati ya tarehe 17 mwezi huu na April 3 nchini Morocco.
Starlets watachuana na Ivory Coast katika mchuano wa pili wa kunoa makali kesho Machi 3, kabla ya kusafiri kuelekea Ufaransa kwa kambi ya mazoezi.
Kenya inarejea katika mashindano ya WAFCON kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2016, na watafungua dimba la WAFCON dhidi ya wenyeji tarehe 17 mwezi huu kundini A kabla ya kumenyana na Senegal na Algeria.