Kundi la Hamas limesema kwamba litamwachilia mateka wa asili ya Israeli na Marekani Edan Alexander, anayeaminiwa kuwa mateka wa mwisho aliye hai raia wa Marekani huko Gaza, kama sehemu ya juhudi za kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Uamuzi huo unajiri kabla ya ziara ya Rais Donald Trump katika eneo la Mashariki ya Kati Jumanne. Hamas imesema hatua hiyo pia inalenga kurahisisha makubaliano ya kuingiza misaada ya kibinadamu. Gaza imekuwa
Mapema, afisa mwandamizi wa Hamas aliambia shirika la BBC kwamba kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina linafanya mazungumzo ya moja kwa moja na afisa wa serikali ya Marekani aliye Qatar.
Afisi ya waziri mkuu wa Israeli ilisema kuwa iliarifiwa na Marekani kuhusu nia ya Hamas ya kumwachilia Alexander.
Afisa mwandamizi wa Kipalestina anayefahamu mazungumzo alisema tangazo la Hamas linalenga kuwa ishara ya nia njema kabla ya kuwasili kwa Trump.
Alisema mkutano mwingine kati ya Hamas na wapatanishi umepangwa kufanyika mapema Jumatatu asubuhi ili kukamilisha mchakato wa kumwachilia Edan, jambo ambalo litahitaji kusitishwa kwa muda kwa operesheni za kijeshi za Israeli na kusimamishwa kwa mashambulizi ya angani wakati wa kumkabidhi.
Rais Trump alithibitisha kuachiliwa kwa Alexander kupitia mtandao wa kijamii wa Truth Social, akitaja tukio hilo kuwa la kihistoria na hatua ya nia njema.
Alexander wa umri wa miaka 21 alizaliwa Tel Aviv lakini akalelewa New Jersey na alikuwa akihudumu katika kituo fulani katika mpaka wa Gaza alipochukuliwa mateka na wapiganaji wa Hamas wakati wa shambulio la Oktoba 7.
Kati ya mateka 251 waliochukuliwa wakati wa shambulio la Hamas la mwaka 2023, 59 wanasemekana kubakia katika eneo hilo, na hadi 24 wanaaminika kuwa hai bado.
Watu watano kati ya mateka walioko Gaza wanaaminika kuwa raia wa Marekani na Alexander anadhaniwa kuwa ndiye pekee aliye hai bado.
Katika taarifa Hamas ilisema kuwa kuachiliwa kwake ni sehemu ya juhudi za kuafikia usitishaji wa mapigano na kuruhusu chakula, dawa na misaada mingine kuingia Gaza.
Afisi ya waziri mkuu wa Israeli ilisema katika taarifa kuwa ilikuwa imearifiwa na Marekani juu ya nia ya Hamas ya kumwachilia Alexander “kama ishara kwa Wamarekani” na kwamba hatua hiyo inatarajiwa kusababisha mazungumzo zaidi juu ya mateka waliobaki.
Sera ya Israel ilikuwa kwamba mazungumzo yatafanywa “katika hali ya vita, kwa kuzingatia dhamira ya kufanikisha malengo yote ya vita”, iliongeza.
Kundi la kampeni la Families and Missing Families Forum limesema kuachiliwa kwa Alexander “lazima kuwe mwanzo wa makubaliano ya kina yatakayohakikisha uhuru wa mateka wote waliobaki”.
Walisema Rais Trump amewapa familia za mateka wote matumaini na kumtaka Netanyahu kuwarudisha wote nyumbani.