Matayarisho yamekamilika kwa mbio za kitaifa za nyika nchini, zilizoratibiwa kuandaliwa kesho mjini Eldoret.
Rais wa Chama cha Riadha Kenya Jackson Tuwei, aliyekagua maandalizi jana katika uwanja wa Eldoret Sports Club, ameelezea kuridhishwa na maandalizi.
Mbio za kesho zitatumika na wanariadha kuwania ubingwa wa kitaifa na pia kwa matayarisho ya mbio za Sirikwa World Cross Country Tour, tarehe 23 mwezi huu katika uwanja wa Lobo, Kapseret.
Mashindano yatang’oa nanga saa nane adhuhuri kwa mbio za kilomita 6 kwa upande wa wasichana chini ya umri wa miaka 20, zikifuatiwa na kilomita 8 wavulana saa saba kasorobo.
Mbio za kilomita 10 wanawake zitaanza saa nane kasoro dakika 20, zikifuatiwa na kilomita 10 wanaume saa moja baadaye.
Mbio za kilomita 2 mzunguko kwa wanaume na wanawake zitakuwa za mwisho saa kumi kasoro dakika 20.
Wanariadha zaidi ya 500 kutoka kote nchini watashiriki.