Hali ya usalama inazidi kudorora katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) huku raia wa kigeni wakianza kutoroka makwao.
Raia kadhaa wa kigeni walionekana jana Jumatano wakitoroka kutoka mji wa Goma mashariki mwa DRC kupitia kwa mpaka wa Rwanda.
Haya yanajiri kufuatia kuongezeka kwa hofu baada ya kundi la waasi wa M23 kuendelea kutwaa maeneo kadhaa muhimu mjini Goma ukiwemo uwanja wa ndege.
Raia wa DRC nao waliendelea na maandamano mjini Kinshasa katika kile kilichoonekana kuwa kupinga serikali za kigeni ambazo wanahisi zinashirikiana na waasi wa M23.
Miongoni mwa walioonekana wakitoroka ni mamluki waliokodiwa na serikali ya Rais Felix Tshisekedi kuwasaidia polisi kudumisha usalama, wengi wao wakiwa raia wa Romania.
Serikali kadhaa za kigeni, zikiwemo Ubelgiji, Marekani, Uingereza, Ufaransa, Uganda, na Rwanda, zimewatahadharisha raia wao kufuatia uvamizi wa balozi mbalimbali siku ya Jumanne.
Marekani imewataka raia wake kuhama nchini DRC pamoja na kutangaza kufunga ubalozi wake.
Marekani pia imetoa ndege za kibinafsi za kusaidia kuwahamisha raia wake.