Hali inazidi kuwa mbaya zaidi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC huku idadi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola ikifikia 5,515 na vifo 2,642.
Visa vipya 51 vimeripotiwa katika mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini, kulingana na takwimu za hivi punde kutoka kwa serikali.
Aidha, serikali imesema kuwa kiwango cha vifo kutokana na ugonjwa huo kimepanda kutoka asilimia 20 mwezi Juni hadi asilimia 48, ambapo yamkini mtu mmoja kati ya wawili wanaoambukizwa hufariki.
Ijumaa iliyopita, DRC ilipokea dozi 16,000 kutoka kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) za chanjo ya Everbo za kuzuia maambukizi ya Ebola, ikiwa sehemu ya dozi 70,000 zinazotarajiwa kuwasilishwa kufikia mapema mwezi ujao.