Hakuna haja ya kuhofu, dawa zipo, Waziri Barasa atoa hakikisho

Martin Mwanje
2 Min Read
Waziri Deborah Barasa akizindua usambazaji dawa kote nchini katika makao makuu ya MEDS

Wizara ya Afya imefutilia mbali hofu ya kuwepo kwa uhaba wa dawa za kutibu magonjwa ya malaria, Virusi vya Ukimwi na kifua kikuu katika kipindi cha angalau mwaka mmoja ujao. 

Hofu hiyo imetokana na hatua ya utawala mpya wa Rais Donald Trump kusitisha ufadhili uliotolewa kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID.

Hatua ya Marekani imelemaza mno utoaji huduma za afya katika mataifa mengi hasa yanayostawi.

Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa anasema licha ya usitishaji huo, hakuna haja ya kuhofu kwa waathiriwa wa magonjwa hayo kwani serikali inafanya kila iwezalo kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu za kutibu magonjwa hayo kila wakati zinapohitajika.

Dkt. Barasa aliyasema hayo leo Ijumaa katika makao makuu ya Shirika la Usambazaji Dawa Muhimu (MEDS) jijini Nairobi. Naye alifika katika makao hayo kuzindua usambazaji wa dawa muhimu hospitalini utakaofanywa na magari zaidi ya 30 kote nchini.

Waziri huyo alielezea kuwa dawa muhimu zinapatikana nchini, ikiwa ni pamja na kondomu za wanaume, ambazo zitadumu kwa kipindi cha takriban miaka miwili ijayo.

Na kufuatia hatua ya Marekani kusitisha ufadhili kupitia USAID, aliongeza kuwa serikali iko mbioni kutafuta ufadhili mbadala kutoka humu nchini.

Kumekuwa na hofu kuwa kujiondoa kwa USAID kutazua janga la afya nchini huku mamilioni ya Wakenya walioathiriwa na magonjwa ya malaria, Ukimwi na kifua kikuu wakiteseka kutokana na ukosefu wa dawa.

Ili kukabiliana na makali ya hatua ya Marekani, serikali sasa imeazimia kushirikiana na MEDS kusambaza dawa muhimu nchini.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *