Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Antonio Guterres kwa mara ya kwanza ametumia kifungo nambari 99 cha mkataba wa umoja wa mataifa, kwenye mzozo wa Gaza.
Kifungo hicho kinasema kwamba, “Katibu mkuu anaweza kufahamisha baraza la usalama kuhusu suala lolote ambalo kwa mtizamo wake linaweza kutishia amani na usalama kimataifa.”
Guterres aliandikia baraza la usalama la umoja wa mataifa waraka Disemba 6, 2023 akitaja mzozo wa Gaza kuwa tishio kubwa kwa amani ulimwenguni.
Alielezea matukio yaliyosababisha mashambulizi yanayotekelezwa na Israel sasa katika ukanda wa Gaza akisema wanamgambo wa Hamas walishambulia Israel Oktoba 7, 2023 na kusababisha vifo zaidi ya 1200.
Kati ya wahasiriwa hao, Guterres anasema kulikuwa na watoto 33 na watu wengine wengi walijeruhiwa huku wengine 250 wakitekwa wakiwemo watoto 34.
Kulingana naye, watu 130 ambao walitekwa nyara Oktoba 7, 2023 na Hamas bado hawajaachiliwa huru hata baada ya kukamilika kwa muda wa kusitisha vita na kuachilia mateka.
Katibu huyo mkuu anataka baraza la usalama la wanachama 15 ambalo ndilo kiungo kilicho na mamlaka makuu katika umoja wa mataifa lichukue hatua kukomesha mapigano huko Gaza.
Kulingana naye baraza hilo bado halijachukua hatua ambayo itasababisha kusitishwa kwa vita na kuokoa maisha na mali ya watu.
Muungano wa Milki za Kiarabu UAE ambao ni mwanachama wa baraza la usalama umejibu waraka wa Guterres ukitaka mapigano yasitishwe kwa sababu za kibinadamu na kwamba imetoa pendekezo lake kwa baraza hilo.