Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, ametoa wito wa mageuzi ya haraka katika Baraza la Usalama la Umoja huo, UNSC na kujumuisha uwakilishi wa mwanachama wa kudumu kutoka bara Afrika.
Amesisitiza kwamba bara hilo halijawakilishwa ipasavyo.
Akihutubia baraza hilo jana Jumatatu, Guterres alisisitiza kuwa muundo baraza hilo unaonyesha uwiano wa mamlaka mwishoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na umeshindwa kuendana na mabadiliko ya dunia.
“Mwaka 1945, nchi nyingi za leo za Kiafrika zilikuwa bado chini ya utawala wa kikoloni na hazikuwa na sauti katika masuala ya kimataifa,” alielezea Guterres.
Aliongeza kuwa haiwezekani baraza hilo linalosimamia masuala ya amani na usalama duniani liwe halina uwakilishi wa bara la Afrika lililo na zaidi ya watu bilioni moja.
“Hatuwezi kukubali kwamba chombo kikuu cha amani na usalama duniani kiwe hakina sauti ya kudumu kwa bara lenye watu zaidi ya bilioni moja na wala hatuwezi kukubali kwamba maoni ya Afrika hayathaminiwi kuhusu masuala ya amani na usalama, katika bara hilo na duniani kote.”
Guterres alisisitiza haja ya kurekebisha mfumo wa Baraza la Usalama akisema, “Kuhakikisha utimilifu na uhalali wa Baraza hili kunamaanisha kutii wito wa muda mrefu kutoka kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, makundi mbalimbali ya kijiografia kuanzia kundi la Waarabu hadi nchi za Benelux, Nordic na CARICOM na baadhi ya wanachama wa kudumu wa Baraza hili lenyewe, kurekebisha dhuluma hii.”
Wanachama 15 wa UNSC wanajumuisha wanachama 5 wa kudumu wenye ushawishi mkubwa wa kura ya turufu ambao ni China, Ufaransa, Urusi, Marekani na Uingereza, huku wanachama wengine 10 wasio wa kudumu wakiteuliwa kwa misingi ya kimaeneo.