Grace Jabbari atupilia mbali kesi dhidi ya Jonathan Majors

radiotaifa
2 Min Read

Mpenzi wa zamani wa mwigizaji wa Hollywood Jonathan Majors, Grace Jabbari ametupilia mbali kesi ya ushambuliaji na kuchafuliwa jina aliyokuwa amewasilisha dhidi ya Majors.

Inaripotiwa kwamba wawili hao waliafikiana nje ya mahakama.

Mawakili wa Majors na Grace Jabbari walikubaliana kwamba kesi hiyo itupiliwe mbali kwa misingi ya chuki bila sababu kulingana na ombi lililowasilishwa katika mahakama ya Manhattan.

Wakili wa Jabbari aitwaye Brittany Henderson alisema kesi hiyo imetatuliwa huku akimsifia mteja wake kwa kudhihirisha ujasiri kwenye mchakato mzima.

Henderson anatumai kwamba mteja wake sasa anaweza kusahau kesi hiyo na kuendelea na maisha yake kwa ujasiri. Mawakili wa Majors hawajatoa taarifa rasmi.

Jabbari aliwasilisha kesi hiyo mwezi Machi ambapo alimlaumu Majors kwa kumdhulumu, kumharibia jina na kumsababishia msongo wa mawazo.

Mcheza densi huyo wa Uingereza aliwasilisha kesi hiyo miezi kadhaa baada ya Majors kuhukumiwa kwa kosa la shambulizi la kiwango cha chini na unyanyasaji kutokana na mvutano wao huko Manhattan.

Mvutano huo ulianzia kwenye gari walilokuwa wameabiri na kuendelea hadi kwenye barabara ambapo Majors anadaiwa kuzaba kofi Jabbari, kupinda mkono wake na kufinya kidole chake cha kati hadi kikaumia.

Majors kwa upande wake alidai kwamba Jabbari ndiye alimshambulia na matendo yake yalikusudiwa tu kupata simu yake na kumwondokea.

Majors alipatiwa hukumu ya kuhudhuria mpango wa ushauri nasaha kwa muda wa mwaka mmoja.

Uamuzi wa mahakama kwamba Majors alikuwa na hatia ulisababisha aachishwe kazi kadhaa za kampuni ya Marvel.

Share This Article