Waakilishi wa Kenya Gor Mahia na Police FC wamesajili matokeo mseto katika mikumbo ya kwanza ya mechi za mataji ya bara Afrika Jumapili jioni.
Gor waliokuwa wakicheza ugenini mjini Juba,walipocharazwa bao moja kwa nunge na El Merreikh Bentiu ya South Sudan katika mchujo wa kwanza mkumbo wa kwanza.
Mohammed Musa alifunga bao la kipekee kunako dakika ya 64.
Matokeo hayo yanawapa Gor shinikizo la kushinda mechi ya marudio kwa mabao mawili kwa bila katika mkumbo wa pili juma lijalo katika uwanja wa Nyayo ili kufuzu kwa mchujo .
Mshindi wa mchujo huo atakumbana na mabingwa wateteziAl Ahly ya Misri katika mchujo wa mwisho.
Wakati uo Police FC wamelazimishwa kutoka sare tasa na Ethiopia Coffee katika mkumbo wa kwanza wa kombe la shirikisho uliosakatwa katika uga wa kitaifa wa Nyayo.
Police FC watasafiri kwenda Addis Ababa Jumapili ijayo kwa mechi ya marudio wakihitaji sare ya magoli ili kufuzu kwa mchujo wa pili watakapomenyana na mabingwa watetezi Zamalek SC ya Misri.
Police wanashiriki mashindano ya Afrika kwa mara ya kwanza.