Gor Mahia wametawazwa mabingwa wa Ligi Kuu Kenya msimu wa mwaka 2023/2024 kwa mara ya 21 kwa jumla. Walitawazwa mabingwa kwa njia ya kipekee baada ya kuwalaza Bidco United mabao 4-3 katika uwanja wa Machakos siku ya Jumapili.
Mfungaji bora msimu huu Benson Omalla alipachika kimiani magoli mawili nao Rooney Onyango na Shaban wakaiongezea Gor goli moja kila mmoja.
John Kelwish pia alifunga magoli mawili kwa wenyeji Bidco huku Jacob Onyango akiongeza la tatu.
Gor wametawazwa mabingwa baada ya kuzoa alama 73, wakishinda mechi 21 kupiga sare 10 na kushindwa mara tatu.
Tusker FC ilimaliza ya pili kwa pointi 65 baada ya kulaza Kakamega Homeboyz bao 1-0 wakifuatwa na Police FC kwa alama 57, baada ya kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Kariobangi Sharks katika mechi ya mwisho.
Bandari imewazima Talanta FC 2-1 ili kumaliza ya nne kwa alama 52, pointi moja zaidi ya AFC Leopards iliyochukua nafasi ya tano baada ya kuwabwaga Ulinzi Stars goli 1-0.
Shabana FC imemaliza ya 14 na kusalia ligini baada ya kuzoa pointi 38 baada ya kuwashinda Muranga Seal 1-0.
Muhoroni Youth na Nzoia Sugar zimeshushwa ngazi huku Sofapaka iliyomaliza ya 16 ikiwa na fursa ya kucheza mechi ya mchujo na timu ya tatu katika ligi ya NSL.
Mathare United na Mara Sugar tayari zimepandishwa ngazi kucheza ligi kuu.
Benson Omalla wa Gor Mahia ameibuka mfungaji bora kwa magoli 19.