Gor Mahia na Police FC watinga mchujo wa pili mataji ya Afrika

Dismas Otuke
2 Min Read
Gor Mahia wakichuana na El Merreikh Bentiu ya Sydan Kusini uwanjani Nyayo

Waakilishi wa Kenya Gor Mahia na Police FC wamefuzu kwa mchujo wa pili wa mataji ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho barani Afrika mtawalia, baada ya kuvuna ushindi Jumapili alasiri.

Gor wakicheza nyumbani kiwarani Nyayo,walilipiza kisasi cha kubanwa golo moja kwa bila katika duru ya kwanza na kuwachachafya El merreikh Bentiu ya Sudan Kusini  mabao 5-1.

Magoli ya mabingwa hao wa ligi ya Kenya mara 21, yametiwa kimiani na Rooney Onyango aliyebusu nyavu mara mbili ,huku Alpha Onyango,Alphonce Omija na Chris Ochieng wakicheka na vya wavu mara moja kila mmoja.

Samuel Akinbinu amefunga bao pekee la kufuta machozi kwa wageni.

Police FC wakipambana na Ethiopian Coffee katika uwanja wa Abebe Bikila mjini Adis Ababa

Mjini Adis Ababa,Ethiopia Police FC, wamesajili ushindi wa bao moja kwa sufuri dhidi ya Ethiopian Coffee  na kufuzu kwa mchujo wa pili kombe la Shirikisho ,bao la maafande likifungwa na Rashid Toha kunako dakika ya 19.

Mechi hiyo imesakatwa katika uga wa Abebe Bikila baada ya duru ya kwanza kuishia sare tasa jijini Nairobi.

Kufuatia matokeo hayo Gor Mahia watakumbana na mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Al Ahly ya Misri katika mchujo wa pili, huku Police FC wakimenyana na mabingwa watetezi wa Kombe la shirikisho Zamalek pia  kutoka Misri.

Gor watawaalika Ahly Septemba 14 kabla ya kuzuru Cairo tarehe 21 mwezi ujao, huku mshindi akifuzu kwa hatua ya makundi.

Police FC pia wataanzia kibarua nyumbani dhidi ya Zamalek tarehe 14 mwezi ujao, kabla ya kuzuru Misri wiki moja baadaye ambapo mshindi wa jumla atatinga hatua ya makundi ya kombe la shirikisho.

Website |  + posts
Share This Article