Gavana Wanga akutana na wahariri anapoandaa kongamano la uwekezaji

Marion Bosire
2 Min Read

Gavana wa kaunti ya Homa Bay Gladys wanga leo asubuhi alifanya mkutano na wahariri wa vyombo mbali mbali vya habari nchini anapoendeleza maandalizi ya kongamano la uwekezaji.

Mkutano huo uliandaliwa kwa lengo la kudurusu namna serikali ya kaunti ya Homa Bay itashirikiana na vyombo vya habari kwa matangazo na mauzo ya kongamano hilo.

Wanga alisema anatambua ushawishi na athari za vyombo vya habari katika kuelekeza maoni ya umma na kuhimiza ushiriki.

“Tunatarajia kushirikiana vyema kwa ajili ya uwekezaji wa siku za usoni katika kaunti ya Homa Bay.” alisema Wanga.

Kongamano la kimataifa la uwekezaji la kaunti ya Homa Bay mwaka 2024 limepangiwa kuandaliwa Februari 27 hadi 29, 2024.

Madhari ya mwaka huu ya awamu hiyo ya pili ya kongamano la uwekezaji la Homa Bay ni “Kufungua ghuba la uwezo sio na mwisho” yaani “Unlocking the Bay of Endless Potential”.

Waandalizi wanalenga kuvutia washiriki wapatao elfu 2 wa mashirika mbali mbali yakiwemo yale ya serikali kuu, wawekezaji wa kitaasisi, wawekezaji wa kibinafsi, serikali za kaunti, taasisi za elimu kati ya wengine.

Awamu ya kwanza ya kongamano la uwekezaji la Homa Bay iliandaliwa Februari 18 na 19 mwaka 2016 katika hoteli ya Tourist huko Homa Bay na gavana wa wakati huo Cyprian Awiti.

Website |  + posts
Share This Article