Gavana wa zamani wa kaunti ya Kiambu Ferdinand Waititu almaarufu “Baba yao” amekamatwa.
Wakili wake Ndegwa Njiru amethibitisha kukamatwa kwa mteja wake kupitia mtandao wa X.
“Mheshimiwa Waititu amekamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI kutokana na matamshi anayodaiwa kutoa akiwa Ruiru Jana,” alidokeza Ndegwa.
Hata hivyo, juhudi za mawakili wa Waititu kuingia katika makao makuu ya DCI kubainisha sababu hasa za kukamatwa kwa Waititu aliyekuwa akihojiwa ziligonga mwamba baada ya kuzuiwa na maafisa wa usalama.
Hali ilikuwa vivyo hivyo kwa viongozi wa upinzani wakiongozwa na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.
Waititu amekuwa akivuta ugwe wa siasa za upinzani tangu alipotalikiana na serikali ya Kenya Kwanza na ameibuka kuwa miongoni mwa wakosoaji wakuu wa utawala huo.