Ni afueni kwa Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo, baada ya hoja ya kumuondoa mamlakani iliyowasilishwa katika bunge la kaunti hiyo kupata kura chache, katika kikao cha Jumanne.
Hoja hiyo iliwasilishwa katika bunge hilo tarehe 26 mwezi Septemba na mwakilishi wadi ya Esise Josiah Mang’era, aliyesema Gavana huyo alikiuka katiba ya Kenya na utumizi mbaya wa mamlaka.
Madai mengine yaliyoibuliwa dhidi ya Gavana huyo, ni pamoja na kuwaajiri wafanyikazi wa kaunti kinyume cha sheria, kupuuza maagizo ya mahakama, kuchelewesha kukamilisha ujenzi wa makao makuu ya kaunti na kutekeleza ukabila wakati wa kuwaajiri wafanyakazi.
Wawakilishi wadi 16 walipiga kura kumfurusha gavana huyo, huku wawakilishi wadi 18 wakipiga kura kupinga kuondolewa kwa Gavana huyo, na hivyo kusitisha wasiwasi uliotanda katika bunge la kaunti hiyo na pia miongoni mwa wakazi wa kaunti hiyo.