Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja, amewahakikishia wakazi wa kaunti hiyo kuwa serikali yake imejitolea kukarabati barabara ambazo zimekuwa katika hali mbaya kwa muda wa miezi kadhaa.
Akizungumza alipofika mbele ya kamati ya uhasibu wa fedha za kaunti na uwekezaji, Gavana huyo alisema baada ya mashauriano, waliafikiana na serikali ya taifa kushughulikia kwa pamoja ukarabati wa barabara hizo.
“Tumekubaliana kushirikiana na serikali ya taifa kushughulikia ukarabati wa barabara. Barabara zingine ziko chini ya serikali kuu huku zingine zikiwa chini ya serikali ya kaunti. Ushirikiano huu utaleta mabadiliko, na hivi karibuni wakazi wa Nairobi watashuhudia mabadiliko hayo,” alisema Sakaja.
Kulingana na Gavana huyo shughuli za ujenzi katika mitaa ya Kilimani na Kileleshwa, zimechangia kuharibika kwa barabara kutokana na malori makubwa ya kubeba vifaa vya ujenzi.
Hata hivyo, alisema wastawishaji hawatapewa leseni za makazi hadi wakarabati barabara zilizoathiriwa wakati wa ujenzi mijengo yao.
“Hali mbaya ya barabara katika mitaa ya Kilimani na Kileleshwa, ni kutokana na shughuli za ujenzi zinazoendelea. Wastawishaji wanafahamu lazima wakarabati barabara hizo watakapomaliza ujenzi wao,” alidokeza Gavana huyo.