Gavana wa kaunti ya Kisumu amefanya mabadiliko katika kamati ya utendaji ya kaunti hiyo ambayo ni sawa na baraza la mawaziri katika serikali ya kitaifa.
Lengo kuu la mabadiliko hayo kulingana na Nyong’o, ni kuboresha utendakazi na utoaji huduma.
Idara muhimu za serikali ya kaunti zimeathiriwa na mabadiliko hayo yaliyomo kwenye stakabadhi iliyotiwa saini na katibu wa kaunti aitwaye Hesbon Hongo.
Paul Waweru amehamishwa kutoka wadhifa wake wa afisa mkuu wa masuala ya fedha na sasa atahudumu kama kaimu afisa mkuu wa shirika la maendeleo ya ufuo wa bahari la Kisumu.
Bovince Ochieng ambaye amekuwa akihudumu kama afisa mkuu anayehusika na masuala ya biashara, vyama vya ushirika na utalii amehamishiwa afisi ya elimu ya kiufundi, uvumbuzi na huduma za jamii.
Erick Omondi ambaye amekuwa akihudumu kama afisa mkuu wa masuala ya kilimi na ufugaji amehamishiwa afisi ya maji, mazingira, maliasili na mabadiliko ya tabianchi.
Francis Asuna ambaye alikuwa akishughulikia masuala ya maji, mazingira na mabadiliko ya tabianchi sasa amehamishiwa afisi ya michezo, jinsia, utamaduni na vijana.
Daniel Otieno ambaye amekuwa akihudumu kama afisa mkuu wa masuala ya nishati, uchukuzi, barabara na ujenzi sasa ni afisa mkuu wa kilimo, maendeleo ya mifugo, uvuvi na uchumi wa majini.
Timothy Nyakwamb Kajwang sasa ndiye afisa mkuu wa masuala Biashara na utalii na awali alikuwa afisa mkuu wa masuala ya michezo, utamaduni na vijana.
Benter Omollo, aliyekuwa akihudumu kama afisa mkuu wa utumishi wa umma sasa atakuwa kaimu afisa mkuu wa masuala ya fedha.
Ojwang Lusi afisa mkuu wa masuala ya afya, Victor Ndereva afisa mkuu wa masuala ya ardhi, Wilson Abiero afisa mkuu wa masuala ya mipango ya kiuchumi, John Oywa afisa mkuu wa mawasiliano wataendelea kuhudumu kwenye nyadhifa zao.
Oywa hata hivyo ameongezewa jukumu la kuwa kaimu afisa mkuu wa masuala ya utumishi wa umma, usimamizi wa kaunti na maendeleo jumuishi.
Mabadiliko hayo yaliyotangazwa jana yalianza kutekelezwa mara moja na yalifanywa na gavana Nyong’o kuambatana na kifungu nambari 45 sehemu ya 5 ya sheria ya mwaka 2012 ya serikali za kaunti.