Gavana wa kaunti ya Laikipia Joshua Irungu ametoa wito kwa bunge kutoingilia fedha zinazotengewa kaunti na tume ya mapato nchini CRA.
Irungu alisema iwapo kiwango cha fedha hizo kitavurugwa na bunge la Senate na lile la taifa, basi miradi ya maendeleo katika kaunti zitaathiriwa.
Kulingana na Gavana huyo, makubaliano ya bunge la Senate na lile la taifa kuhusu kupunguzwa kwa mgao kwa kaunti wa mwaka 2024/25 kutoka shilingi bilioni 400 hadi shilingi bilioni 380, utasababisha kaunti ya Laikipia kupotesha shilingi milioni 250.
Kwa upande wake, kamishna wa tume ya CRA Isabella Waiyaki, alipongeza kaunti ya Laikipia kwa kuwa miongoni mwa kaunti ambazo zimeimarisha ukusanyaji wa mapato.
Alisema tangu kuanzishwa kwa ugatuzi, kaunti ya Laikipia imeongeza mapato yake kutoka shilingi milioni 300 hadi shilingi bilioni 1.1 kila mwaka.
Isabella alisema iwapo kaunti zitaimarisha uwezo wa kukusanya mapato, basi zitapunguza hali ya kutegemea mapato kutoka kwa serikali kuu.
Viongozi hao wawili walizungmza leo mjini Rumuruti, wakti wa mkutano kuhusu kuimarisha uwezo wa kaunti kukusanya ushuru.