Gavana Barasa kulipa bili za waathiriwa wa maandamano Kakamega

Tom Mathinji
1 Min Read
Gavana wa KakamegaFernandes Barasa, asema serikali yake itagharamia bili za hospitali kwa wahasiriwa wa maandamano.

Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, amesema serikali ya kaunti hiyo itagharamia malipo ya matibabu na kwa  waathiriwa wa maandamano yaliyopinga Mswada wa Fedha 2024.

Barasa aliyeomboleza na familia zilizowapoteza wapendwa wao, alisema serikali yake pia itagharamia mazishi ya waliofariki wakati wa maandamano hayo.

Kulingana na Barasa, serikali hiyo itagharamia mazishi ya  Caroline Ashirambo kutoka ikolomani na Richard Ouko kutoka kaunti ya  Kisumu, waliofariki wakati wa maandamano hayo.

Aidha, alikashifu utumizi wa nguvu kupita kiasi na maafisa wa polisi, hususan utumizi wa risasi dhidi ya waandamanaji.

Akizungumza alipowatembelea wahasiriwa hao katika hospitali ya rufaa ya Kakamega, Gavana Barasa alitangaza kuwa wavulana wawili wa umri wa miaka 22 na 19 hawatatozwa malipo yoyote ya kutibiwa katika hospitali hiyo.

Akitoa rambi rambi zake kwa familia zao,Barasa alidokeza kwamba serikali ya kaunti hiyo pia ilipata hasara kubwa baada ya baadhi ya afisi zake na magari yake 18 kuteketezwa.

Alitoa wito kwa vijana wanaofahamika kama Gen Z, kushiriki maandamano ya amani.

Website |  + posts
Share This Article