Gavana Barasa ataka maafisa wafisadi NHIF waadhibiwe vikali

Martin Mwanje
2 Min Read
Gavana wa kaunti ya Kakamega, Fernandes Barasa.

Gavana wa kaunti ya Kakamega Fernandes Barasa ametoa wito kwa Rais William Ruto kuwachukulia hatua kali maafisa wafisadi katika Hazina ya Bima ya Kitaifa, NHIF. 

Kumekuwa na madai ya matumizi mabaya ya mamilioni ya fedha katika hazina hiyo katika siku za hivi karibuni.

Hata hivyo, Barasa ameonya kuwa ni raia watakaobeba mzigo wa madhara ya uongozi mbaya kwenye hazina hiyo.

Gavana huyo aliyasema hayo alipowahutubia wazazi, walimu na wanafunzi wa sasa na wa zamani wa shule ya St. Mary’s Mumias wakati wa maadhimisho ya miaka 50 tangu kuasisiwa kwa shule hiyo.

Kauli zake zinakuja wakati ambapo Kamati ya Afya ya Bunge imetangaza kuwa itaanzisha uchunguzi wa umma kuhusu madai ya matumizi mabaya ya fedha kwenye hazina ya NHIF.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni mbunge wa Endebess Robert Pukose, akizungumza baada ya kukutana na uongozi mkuu wa hazina hiyo juzi Jumanne, alisema ni uchunguzi wa kina tu utakaofichua ukweli kuhusu udanganyifu mkubwa wa fedha kwenye NHIF akiongeza kuwa wakati umewadia wa  kuifanyia hazina hiyo mabadiliko makubwa.

“Sisi kama kamati hatuwezi tukakimya wakati kuna madai ya matumizi mabaya ya fedha ndani ya NHIF. Njia pekee ya kubaini ukweli na kupitia uchunguzi wa umma,” alisema Pukose.

“Wiki ijayo, tutafanya mkutano kubuni miongozo ya uchunguzi huo na kuwaalika washikadau wote husika kuwasilisha uelewa wao wa hali ilivyo katika NHIF.”

Sehemu ya uchunguzi huo itaangazia madai ya kupendelewa kwa hospitali za kibinafsi ikilinganishwa na zile za umma.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *