Gavana wa kaunti ya Kwale amesema kuwa ataendeleza juhudi za kuboresha miundombinu ya manispaa ya Lungalunga katika mikakati ya kukuza biashara na uchumi katika eneo hilo lililo katika mpaka wa Kenya na Tanzania.
Manispaa ya mji huo ulioko takriban kilomita 6 kutoka kwa mpaka wa Kenya na Tanzania, iliidhinishwa rasmi na Gavana Fatuma Achani tarehe 11 Julai, 2022, ikiwa kivutio kikubwa cha biashara kati ya wakazi wa mji huo na wenyeji wa nchi jirani ya Tanzania na kufikisha idadi ya manispaa kuwa 4 ikiwemo Kwale, Diani, Kinango na Lungalunga.
Akizungumza alipokuwa akizindua ukarabati wa barabara ya Ziwani kuelekea kwenye Soko la Lungalunga, Gavana Achani amewahimiza wakazi wa eneo hilo kushirikiana na serikali yake katika juhudi za kuupandisha hadhi mji huo, akisema kuboreshwa kwake kutasaidia kukuza uchumi wa kaunti kupitia biashara.
Kiongozi huyo aidha ameahidi kutafuta suluhu ya kudumu kutokana na suala tata la ukosefu wa maji katika mji huo, akisema kwa muda mrefu, suala hilo limekuwa likitatiza shughuli mbalimbali zinazoendelea kwenye mji huo.