Huku msimu wa mvua za masika ukitarajiwa kuanza hivi karibuni, Serikali ya Kaunti ya Kwale imezindua ugavi wa mbegu za mahindi, pojo na kunde kwa wakulima wa kaunti hiyo.
Hatua hiyo inalenga kuboresha uzalishaji mazao ya kilimo katika Kaunti ya Kwale.
Jumla ya tani 39 za mbegu zimetolewa kwa wakulima 15,000, huku tani 23 zikiwa za mahindi, 8 za pojo na zingine 8 zikiwa za kunde.
Kaunti ya Kwale imekuwa ikitoa mbegu kwa wakulima kwa miaka 12, huku zaidi ya tani 400, zikitolewa na wakulima 180,000 wakifaidika.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo katika Makao Makuu ya Kaunti hiyo, Gavana wa Kwale Fatuma Achani, alisema serikali ya Kwale inahakikisha kuwa sekta ya kilimo inaangaziwa ili kuwezesha uzalishaji wa chakula cha kutosha Kaunti hiyo.
Kauli za Gavana huyo zimeungwa mkono na Mwakilishi Wadi wa Tsimba Golini Mwachuo Mwaboza na Waziri wa Kilimo wa Kaunti ya Kwale Roman Shera, waliowataka wakulima kuzingatia mafunzo kutoka kwa maafisa wa kilimo wa Kaunti hiyo.