Gavana Achani afungua kiwanda cha kusaga mihogo Kwale

Martin Mwanje
1 Min Read

Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) amefungua rasmi kiwanda cha kuchambua, kukausha na kusaga mihogo katika kaunti hiyo. 

Kiwanda hicho kipo katika kijiji cha Magodi, wadi ya Ramisi katika eneo bunge la Msambweni.

Kiwanda hicho chenye uwezo wa kusaga takriban tani moja ya unga wa mihogo kwa siku, kilianzishwa mnamo mwaka wa 2021 ili kukuza kilimo cha mihogo katika kaunti ya Kwale.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Achani amesema serikali yake itashirikiana na washikadau mbalimbali katika sekta ya kilimo, ili kuhakikisha kuwa miradi ya kilimo inanawiri na kuleta maendeleo kwa wenyeji wa kaunti hiyo na kukuza uhumi wa kaunti ya Kwale.

Kwa upande wake, mjumbe wa EU humu nchini Alexander Baron amewataka wakazi wa Kwale kutumia nafasi ya ujio wa kiwanda hicho kujinufaisha kimaisha na kuongeza mapato ya kaunti hiyo.

Wakulima wakiongozwa na Ann Kiswii, wameshukuru ujio wa kiwanda hicho cha mihogo, wakisema kimewapa nafasi nyingi za ajira kupitia kilimo cha zao hilo.

Share This Article