Naibu Rais Rigathi Gachagua ametoa ahadi kwa Waziri wa kilimo Dkt. Andrew Karanja na mwenzake wa Ustawi wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya kuwa atawasaidia kuhakikisha taifa hili linashuhudia ongezeko la uzalishaji chakula na kuimarika kwa mapato ya wakulima.
Gachagua aliwaambia mawaziri hao wawili kuwa atashirikiana nao kwa karibu, kuhakikisha serikali inatimiza ndoto yake katika sekta ya kilimo.
Akizungumza wakati wa mkutano kati ya wizara mbali mbali afisini mwake katika mtaa wa Karen, Nairobi, naibu huyo wa Rais alitoa wito kwa mawaziri hao kuwahusisha wakulima katika ajenda ya mageuzi.
Alisema serikali inalenga kurekebisha sera, mbinu endelevu na kutafuta soko la mazao.
“Usalama wa chakula ni miongoni mwa nguzo za Kenya Kwanza, na ninawasihi kuhakikisha serikali inafanikiwa. kwa pamoja tuunde uchumi imara. Ikiwa wizara hizo zitafanya kazi pamoja, hali itabadilika kwa urahisi. Nitawasaidia kwa chochote mtakachotaka,” alisema Gachagua.
Kuhusu sekta ya majani chai, Gachagua aliwasihi wakurugenzi wapya waliochaguliwa wa halmashauri ya ustawi wa majani chai nchini KTDA, kuonyesha uongozi bora kwa kupunguza gharama ya uzalishaji katika viwanda.
“Tunatumia fedha nyingi kwa uzalishaji. Lazima tukubalieni kuhusu gharama ya uzalishaji….kama serikali tuko tayari kuwasaidia kuleta uthabiti katika halmashauri ya KTDA,” alisema naibu huyo wa Rais.
Alisema uzalishaji wa kahawa ulipungua kutokana na usimamizi mbaya wa vyama vya ushirika.
“Sekta ya kahawa imekumbwa na matatizo kwa muda wa miongo miwili…. tunazijatiti kuongeza uzalishaji, kuimarisha bei na kuwapa wakulima motisha wa kurejelea kilimo cha kahawa,” alidokeza Gachagua.
Gachagua aliwahimiza wabunge kubuni sheria zitakazosaidia serikali kutimiza ajenda zake katika sekta ya kilimo.