Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema amefaulu katika ajenda ya kuleta mageuzi katika sekta ya kahawa, huku akiwapuuzilia mbali wakosoaji wake.
Gachagua aliyasema hayo siku ya Ijumaa alipozuru viwanda vya kahawa katika kaunti ya Kiambu kukagua maendeleo kuhusi mageuzi hayo.
Naibu huyo wa Rais alitaja ufanisi ulioshuhudiwa katika kiwanda cha kahawa cha Gathiru-ini, ambapo wanachama wake walilipwa shilingi 87 kwa kila kilo moja ya kahawa mwaka huu, hii ikiwa ni ongezeko la shilingi 13.
“Ninafuraha kutokana na mageuzi katika sekta ndogo ya kahawa. Bei iliyoimarika katika kiwanda cha kahawa cha Gathiru-ini, ni ishara tumefaulu katka ajenda ya mageuzi. Kiwanda hicho kinalenga kununua kilo moja ya kahawa shilingi 110 na baadaye shilingi 150. Wale ambao wanatukosoahawaelewi sekta hii na huwa hawajihusishi na kilimo,” alisema Gachagua.
Gachagua aliyekuwa ameandamana na baadhi ya viongozi wa kisiasa, alitoa wito kwa wabunge kupitisha kwa haraka mswada wa kahawa wa mwaka 2023 na ule wa vyama vya ushirika wa mwaka 2023, ili kuwakinga wakulima dhidi ya madeni na kuhadaiwa na mawakala.
“Miswada hiyo miwili inalenga kuwafaidi wakulima na kulainisha usimamizi wa vyama vya ushirika. Tunanuia kufufua bodi ya kahawa nchini na taasisi ya utafiti wa kahawa, ili kuwawezesha wakulima kupata aina bora za kahawa,” alidokeza Gachagua.
Alitoa wito kwa vijana kuwania uongozi katika vyama vya ushirika vya kahawa.
Naibu huyo wa Rais alizuru kiwanda cha kahawa cha Gathiru-ini, na baadaye aliungana na wakulima wa chama cha ushirika cha wakuliwa wa kahawa cha Komothai kwa mkutano mkuu wa kila mwaka.