Seikali imekusudia kutekeleza mabadiliko sahihi katika sekta ya majani chai kupitia mtazamo unaotoa kipaumbele kwa wakulima.
Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema mabadiliko yanayoshinikizwa yatahakikisha wakulima wanavuna manufaa mengi wakati wakiendelea kuunga mkono uchumi wa nchi.
“Sekta ya kilimo inachangia asilimia 22 ya Pato Ghafi la Kitaifa, huku sekta ya majani chai ikichangia asilimia 2. Huku kukiwa na zaidi ya wakulima 650,000 waliopo katika kaunti 18, Kenya ni nchi inayoongoza katika uzalishaji na uuzaji nje ya nchi wa majani chai ya aina mbalimbali, majani chai meusi yakichangia angalau asilimia 95 ya majani yanayouzwa,” alisema Gachagua.
“Tunataka mkulima wa majani chai kuonekana mrembo jinsi mandhari ya mashamba ya majani chai yanavyopendeza. Lazima tupate suluhu. Mkulima lazima apate faida kubwa katika mazungumzo haya ya mwisho kuhusu majani chai.”
Gachagua aliyasema hayo leo Alhamisi wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku tatu wa mabadiliko ya majani chai katika kaunti ya Kericho.
Aliwasihi wakulima kukumbatia teknolojia na pia uongezaji wa thamani akisema vyote hivyo vitaimarisha sekta hiyo pakubwa.
Mkutano huo unalenga kutoa jukwaa kwa wakulima wa majani chai kuangazia changamoto zinazoikumba sekta hiyo na kutafuta njia za kuzisuluhisha.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Waziri wa Kilimo Mithika Linturi alisema wakati umewadia wa kuweka tabasamu kwenye nyuso za wakulima.
“Kenya inazalisha majani chai bora duniani, lakini haiwezi ikavutia bei bora kwa ajili ya wakulima wetu. Ni sharti tuwazie namna ya kunufaika na majani chai yetu na kupata mapato ya juu zaidi,” alisema Linturi.
Seneta wa kaunti ya Kericho Aaron Cheruiyot aliunga mkono mkutano huo akisema utasaidia kujumuisha mabadiliko yaliyopendekezwa ili kuiboresha sekta hiyo.