Naibu Rais Rigathi Gachagua, leo anatarajiwa kuzindua mfumo wa kidijitali ya kusimamia usafiri nje ya nchi wa maafisa wa serikali na mfumo wa maelekezo ya Rais.
Uzinduzi huo utafanyika katika jumba la KICC jijini Nairobi.
Mkuu wa utumishi wa umma Felix Koskei alitangaza ujio wa majukwaa hayo mawili awali akisema kwamba lengo kuu ni kuimarisha uwazi katika utumishi wa umma na kupunguza gharama ya usafiri.
Jukwaa la maelekezo ya Rais kwa upande mwingine linalenga kuorodhesha maelekezo hayo na kunakili viwango vya utekelezaji wake ili kuhakikisha uwajibikaji.
Kulingana na Koskei jukwaa la safari za nje almaarufu Foreign Travel Management System – FOTIMS litatumiwa na waajiriwa wote wa serikali wanaotafuta kusafiri nje.
Mfumo huo utasaidia pia kuhakikisha kwamba mchakato wa kuidhinisha safari hizo umelainishwa huku wafanyakazi husika wa serikali wakiweza kujipanga sawasawa kwa safari zao.
Utasaidia pia katika kuhakikisha kwamba sera za usafiri nje ya nchi zinafuatwa na wafanyakazi wa serikali na kuboresha maamuzi kupitia utathmini wa deta.
Mfumo wa maelekezo ya Rais au ukipenda Presidential Directives Management Information Systems – PDMIS nao utatumiwa kutoa maelekezo ya Rais kwa wafanyakazi wa serikali.
Wahusika wa utekelezaji wa maelekezo hayo wakiwemo mawaziri na makatibu wa wizara wataweza kushusha nakala za maelekezo hayo kutoka kwenye tovuti hiyo ili kuyashughulikia.