Gachagua kushawishi upinzani kutoka Mlima Kenya kujiunga na serikali

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema ataanzisha juhudi za kuwashawishi viongozi wa muungano wa Azimio la Umoja katika eneo la mlima Kenya kujiunga na upande wa serikali.

Akizungumza katika kaunti ya Meru siku ya Jumamosi wakati wa mazishi ya kakake mbunge wa Tigania Mashariki Mpuri Aburi, Gachagua alisema mchakato huo ukifanikiwa, siasa za kutengwa kimaendeleo katika eneo hilo zitamalizwa.

Gachagua aliwakosoa viongozi wa eneo hilo, wanaopinga juhudi hizo za kuunganisha eneo nzima la mlima Kenya.

Naibu huyo wa Rais alidokeza kuwa atajizatiti kuwashawishi aliyekuwa Gavana wa eneo hilo Peter Munya na mbunge wa Igembe kaskazini Maoka Maore, kujiunga na serikali.

Peter Munya aliunga mkono uwaniaji wa Urais wa Raila Odinga, katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Maoka Maore kwa upande wake aliwania kiti cha ubunge cha Igembe Kaskazini kupitia tiketi ya chama cha Jubilee.

Kulingana na Gachagua, mpango huo ukifaulu, utapiga jeki azma ya Rais William Ruto ya  kuchaguliwa tena katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Ziara ya Gachagua katika kaunti ya Meru inajiri huku wawakilishi wadi wa kaunti hiyo wakianzisha mchakato wa kumng’oa Gavana Kawira Mwangaza mamlakani.

Website |  + posts
Share This Article