Naibu Rais Rigathi Gachagua, leo Ijumaa atazuru kaunti ya Kiambu, kukagua marekebisho yanayotekelezwa katika sekta ndogo ya kahawa.
Ziara ya Gachagua itaanzia katika chama cha ushirika cha Komothai, ambapo atahudhuria Mkutano Mkuu wa kila mwaka wa chama hicho.
Chama hicho cha ushirika cha Komothai, kinachojumuisha viwanda vya kahawa vikiwemo; Riakahara, Gathiru-ini, Barikongo, Kagwanja, Kirura, Korokoro, Githongo, Thiururi, Kaibu, New Thuita, Kanake, Gatuyu na Kamuchege, ni mojawepo wa vyama vikuu vinavyomilikiwa na wakulima wadogo wadogo wa kahawa.
Baadaye naibu huyo wa Rais, atazuru kiwanda cha kahawa cha Gathiru-ini na kile cha Kigumo, kukagua operesheni zake, kabla ya kuwahutubia wakulima wa kahawa kuhusu mageuzi yanayotekelezwa katika sekta hiyo.
Gachagua amejukumiwa kuongoza mageuzi katika sekta ndogo ya kahawa, huku akiongoza kamati inayotekeleza marekebisho hayo.
Serikali ya Kenya kwanza, iliahidi kufanyia mageuzi sekta ndogo ya kahawa, kuhakikisha wakulima wanafaidika kutokana na ukuzaji wa zao hilo.