Gachagua, Kindiki wakutana wakati ubabe wa kisiasa ukirindima kati yao

Martin Mwanje
2 Min Read

Naibu Rais Rigathi Gachagua na Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki wamekutana ana kwa ana leo Jumanne tangu kuibuka kwa ubabe wa kisiasa kati yao. 

Wawili hao walikutana wakati wa mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi na kuongozwa na Rais William Ruto.

Gachagua na Prof. Kindiki wamo mbioni kupigania ubabe wa siasa za Mlima Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Awali, Gachagua aliashiria kuwa yeye ndiye kigogo wa siasa za Mlima Kenya.

Hata hivyo, kundi la wanasiasa kadhaa wa Mlima Kenya lilijitokeza siku chache zilizopita na kutangaza kuwa wanamuunga mkono Prof. Kindiki kuwa kigogo wa siasa za Mlima Kenya.

Ni hali ambayo imesababisha kuchipuka kwa mirengo miwili ya kisiasa katika eneo la Mlima Kenya, mmoja ukimshabikia Gachagua na mwingine Prof. Kindiki.

Siku zilizopita, kulikuwa na madai kuwa makali ya mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro yananolewa ili kuchukua mahali pa Gachagua katika uchaguzi wa mwaka 2027.

Gachagua ametofautiana na Rais Ruto kiasi kwamba hakuhudhuria mkutano mkubwa wake ulioandaliwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika kaunti ya Nyeri.

Kiti cha Naibu wa Rais kilisalia wazi wakati wa hafla hiyo ambayo pia ilihudhuria na Gavana wa kaunti ya Nyeri Mutahi Kahiga.

Kahiga ni mfuasi sugu wa Naibu Rais.

Share This Article