Naibu Rais aliyebanduliwa madarakani Rigathi Gachagua kwa mara nyingine amepata pigo mahakamani.
Hii ni baada ya jopo la majaji watatu Mahakama Kuu kuondoa maagizo yaliyozuia kuapishwa kwa Naibu Rais mteule Prof. Kithure Kindiki.
Hatua hiyo inamaanisha kuwa Prof. Kindiki yuko huru kula kiapo cha kuhudumu katika wadhifa huo.
Kulikuwa na ripoti kuwa Prof. Kindiki huenda akaapishwa kesho Ijumaa.
Katika uamuzi wao, Majaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Dkt. Freda Mugambi wamesema katiba ya mwaka 2010 haukitazamia kuwepo kwa ombwe katika afisi ya Naibu Rais.
Isitoshe, majaji walisema majukumu ya Naibu Rais hayawezi yakatekelezwa na mtu mwingine yeyote kwa mujibu wa kifungu cha 147 cha katiba na itakuwa bora nafasi hiyo kujazwa kutokana na maslahi ya umma.
Ni kwa Kwa misingi hiyo, majaji hao wamekatalia mbali ombi la Gachagua la kuitaka mahakama kumpa maagizo ya kuzuia kuapishwa kwa mrithi wake.
Aidha, mahakama imefutilia mbali maagizo yaliyotolewa na mahakama ya Kerugoya yaliyozuia kuapishwa kwa Prof. Kindiki.
Katika uamuzi wao, majaji walisema wataendelea kusikiliza kesi ya Gachagua wakati Prof. Kindiki akihudumu kama Naibu Rais, na ikiwa mwishoni mwa kesi hiyo, itabainika kuwa utaratibu mwafaka haukufuatwa katika kumfurusha Gachagua, basi mahakama itatoa maelekezo kuhusiana na suala hilo.
Gachagua amekuwa akipigana kwa udi na uvumba kuzuia kuapishwa kwa Prof. Kindiki kama Naibu Rais ila katika kila maamuzi ambayo yametolewa, ameonekana kuibuka mshinde.
Mahakama ilimpa Gachagua uhuru wa kukataa rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Awali, Mahakama ya Rufaa ilikataa kutoa maagizo ya kuzuia jopo hilo la majaji watatu kutoa uamuzi juu ya maagizo yaliyozuia kuapishwa kwa Prof. Kindiki.