Gachagua akata rufaa kupinga kusikizwa kwa kesi za kubanduliwa kwake

Martin Mwanje
2 Min Read

Naibu Rais Rigathi Gachagua amekata rufaa kupinga kusikizwa kwa maombi mawili ya kutaka maagizo ya kuzuia kubanduliwa kwake madarakani yafutiliwe mbali.

Jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu ambao ni Eric Ogola, Athony Mrima na Dkt. Freda Mugambi limepangiwa kuanza kusikiza maombi hayo kesho Jumanne.

Katika kesi ya dharura aliyoiwasilisha katika Mahakama ya Rufaa leo Jumatatu, Gachagua anataka majaji hao kuzuiwa kusikiza maombi hayo.

Ikiwa jopo la majaji hao litaondoa maagizo hayo, basi hatua hiyo itatoa fursa ya kuapishwa kwa mrithi wa Gachagua Prof. Kithure Kindiki.

Gachagua pia amekata rufaa dhidi ya uamuzi wa majaji hao kuwa Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu alikuwa na mamlaka ya kuwateua kusikiza kesi ya kupinga kubanduliwa kwake.

Kupitia kwa mawakili wake wakiongozwa na Paul Muite, Gachagua alisema wajibu wa kuwateua majaji umetengewa Jaji Mkuu.  Kulingana naye, majaji hao walikosea katika kuifasiri katiba.

Juhudi za Gachagua za kuwataka majaji Ogola, Mrima na Dkt. Mugambi kujiondoa kwenye kesi hiyo ziliambulia patupu baada ya wao kukataa kujiondoa.

Naibu Rais huyo aliyebanduliwa madarakani na Bunge la Seneti aliwataka majaji hao kujiondoa akidai wana uhusiano na upande wa washtakiwa na kwa misingi hiyo watakuwa na upendeleo.

Hadi kufikia sasa, majaji hao wametoa uamuzi mara mbili ambao umekuwa pigo kwa Gachagua katika juhudi zake za kutaka kuendelea kuhudumu kama Naibu Rais wa nchi.

Share This Article