Gachagua akanusha madai ya kuwachochea wafanyabiashara Nairobi

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Naibu Rais Rigathi Gachagua amejitetea dhidi ya madai kwamba aliingilia uongozi wa serikali ya kaunti ya Nairobi, kwa kuwachochea wafanyabiashara dhidi ya maagizo yaliyotolewa na kaunti hiyo.

Kulingana na Gachagua, mkutano wake na wafanyabiashara hao Septemba 29, ulitokana na kilio chao kwamba hakikushughulikiwa na serikali ya kaunti ya Nairobi.

“Niliposhiriki mkutano wa hadhara na wanabiashara hao, nilikuwa namsihi Gavana wa Nairobi kusikiliza kilio cha wanabiashara hao. Nitatoa ushahidi wa video Jumanne katika bunge la taifa,” alisema Gachagua.

Gachagua alisema wanabiashara hao walimtaka aingilie kati ili kusuluhisha matatizo yao, na kile alichofanya ni kumshauri Gavana wa kaunti hiyo kuwasikiliza kuhusiana na swala la kuwahamisha hadi kwa soko jingine.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alikuwa ameagiza baadhi ya wanabiashara katika soko la Wakulima wahamishwe hadi katika soko lililoko kwenye barabara ya Kangundo, hatua ambayo wafanyabiashara hao walipinga vikali.

Naibu huyo wa Rais alikuwa akizungumza Jumatatu jioni katika makazi yake rasmi ya Karen, kujibu madai yaliyolimbikizwa dhidi yake katika hoja iliyowasilishwa bungeni na mbunge wa Mwingi Magharibi Mwengi Mutuse ya kumbandua mamlakani.

Gachagua alithibitisha kuwa atafika mbele ya bunge la taifa kujitetea dhidi ya madai hayo saa kumi na mpja jioni.

Share This Article