Gachagua akana mashtaka yote 11 katika Bunge la Seneti

Martin Mwanje
1 Min Read
Naibu Rais Rigathi Gachagua akiwa katika Bunge la Seneti

Naibu Rais Rigathi Gachagua amekana mashtaka yote 11 yaliyowasilishwa dhidi yake katika Bunge la Seneti kwa lengo la kumbandua madarakani.

Gachagua alisomewa mashtaka hayo na Karani wa bunge hilo Jeremiah Nyegenye mwanzoni mwa kikao cha kuyasikiza.

Kikao hicho cha Maseneta wote kitaendelea hadi kesho Alhamisi.

Mashtaka hayo ni pamoja na matumizi mabaya ya rasilimali za umma, kujilimbikizia mali kupitia njia za kutilia shaka, kueneza semi za chuki, ukabila na kumhujumu Rais.

Naibu Rais sasa atapewa muda wa kujitetea mbele ya Maseneta kuhusiana na mashtaka hayo.

Bunge la Seneti linaandaa kikao hicho kufuatia kupitishwa kwa hoja maalum ya kumtaka Gachagua kutimuliwa madarakani.

Hoja hiyo iliwasilishwa katika Bunge la Taifa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.

Hoja hiyo ilipitishwa na wabunge 281 huku 44 wakiipinga.

Awali, Gachagua alipata pigo baada ya jopo la majaji watu wakiongozwa na Eric Ogola kukataa kuzuia Seneti kusikiza mashtaka dhidi yake.

 

Website |  + posts
Share This Article