Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amemshauri Rais William Ruto kufutilia mbali Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA ambayo imejukumiwa kusimamia bima mpya ya matibabu ya SHIF kwa kukosa mwelekeo.
Ameongoza kuwa licha ya bima ya SHIF kuanza kutekelezwa mwezi mmoja uliopita, bado Wakenya wengi hawajaanza kunufaika na badala yake wanahangaishwa kila wanapotafuta huduma za matibabu.
Kalonzo amempongeza Rais kwa kufutilia mbali mikataba miwili na kampuni yenye utata ya Adani, ukiwamo ule wa Ketraco na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JKIA, baada ya Adani kukabiliwa na kashfa za kutoa hongo nchini India ili kupata zabuni.
Kiongozi huyo wa Wiper pia amependekeza kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wale wote waliohusika katika kutia saini mikataba hiyo miwili.