Filamu ya Celine Dion kuzinduliwa

Marion Bosire
1 Min Read

Kampuni ya kuandaa na kusambaza video na filamu Amazon MGM Studios imetangaza ujio wa filamu ya matukio halisi kuhusu mwanamuziki Celine Dion.

Filamu hiyo kwa jina “I Am Celine Dion” haitagusia maisha yote ya mwimbaji huyo bali itaangazia kipindi cha mwaka mmoja hivi ambapo amekuwa akipambana na maradhi yasiyo ya kawaida.

Kwa muda sasa, Dion amekuwa akiugua ugonjwa unaoathiri mfumo wa neva mwilini almaarufu “Stiff Person Syndrome”.

Maradhi hayo yanayoathiri ubongo na uti wa mgongo yamesababisha mwanamuziki huyo kushindwa kuendeleza kazi zake.

Anatumai kwamba ataweza kuhamasisha watu kuhusu ugonjwa huo kupitia kwa filamu hiyo ambayo itapatikana kwenye jukwaa la filamu na video mitandaoni kwa jina Amazon Prime Video.

Tarehe kamili ya uzinduzi wa kazi hiyo haijatangazwa.

Disemba 2022 ndio wakati Celine Dion alitoa habari kuhusu kuugua kwake na Mei 2023 akalazimika kusitisha tamasha ambazo alikuwa amepanga kwani hakuwa na uwezo wa kutumbuiza.

Dion anasema sasa ameelewa kwamba maradhi hayo ndiyo yamekuwa yakimsababishia hali ya kunywea ghafla kwa misuli.

Share This Article