FIDA yashutumu mauaji ya wanawake nchini

Martin Mwanje
1 Min Read

Chama cha Mawakili Wanawake, FIDA imeshutumu vikali visa vinavyoongezeka vya mauaji ya wanawake  nchini kwa sasa.

Kinasema hadi kufikia sasa, jumla ya wanawake 30 wameuawa na wapenzi wao mwaka huu, mauaji ambayo yalitokana na dhuluma za kinyumbani.

Chama hicho sasa kinamtaka Rais William Ruto kuingilia kati na kusaidia kupaza sauti za kutaka mauaji hayo kukomeshwa mara moja.

“Mauaji ya wanawake ni dharura ya kitaifa ambayo inahitaji ofisi kuu kuingilia kati,” walisema viongozi wa chama hicho wakati wakiwahutubia wanahabari leo Jumanne.

Miongoni mwa matakwa yake, FIDA inataka mauaji ya wanawake kutangazwa kuwa janga la taifa, polisi kuamrishwa kutoa taarifa ya kina juu ya suala hilo katika kipindi cha siku saba zijazo na Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuelezea hadhi ya uchunguzi wa washukiwa wote ikiwa ni pamoja na mshukiwa mkuu wa mauaji ya eneo la Kware, Embakasi Mashariki Collins Jumaisi.

Rais Ruto pia ametakiwa kujaza haraka wadhifa wa Waziri wa Jinsia.

 

 

Website |  + posts
Share This Article