Serikali imelainisha mifumo yake ili kukomesha uchelewashwaji wa fedha za Hazina ya Inua Jamii, kwa mujibu wa Katibu katika Idara ya Uhifadhi wa Jamii Joseph Motari.
Fedha za hazina hiyo huwanufaisha wazee, watu wenye ulemavu na watoto mayatima.
Motari amefichua kuwa fedha hizo sasa zitatolewa tarehe 15 kila mwezi kufuatia amri ya Rais William Ruto.
Hii ni baada ya serikali kuchelewa kutoa fedha hizo kwa kipindi cha miezi minane na kuibua vilio kwa watu wanaonufaika nazo wanaozitegemea kukidhi mahitaji muhimu ya kila siku.
Akizungumza mjini Thika wakati wa utoaji wa viti vya magurudumu na vifaa vingine vya kuwasaidia watu wenye ulemavu vilivyotolewa na shirika lisilokuwa la serikali la Hope Mobility Kenya kwa watu wenye ulemavu zaidi ya 300, Motari alisema ucheleweshaji wa fedha hizo unawaathiri wanaonufaika na fedha hizo hasa watu wenye ulemavu.
Alidokeza kuwa serikali imeanzisha mpango wa kuwasajili watu zaidi wenye ulemavu, wazee na mayatima katika mpango huo.