FAO, WFP zasaini makubaliano ya kushirikishana taarifa Somalia

Martin Mwanje
2 Min Read
29 November 2021, Rome, Italy - FAO members' flags are hoisted outside the Food and Agriculture Organisation of the United Nations Headquarters on the occasion of the FAO Council 168th Session opening, FAO Headquarters.

Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) yamesaini makubaliano ya kushirikishana taarifa mjini Mogadishu nchini Soamlia.

Mashirika hayo mawili ya Umoja wa Mataifa, UN yanawahudumia mamilioni ya watu wasiojiweza nchini Soamlia kupitia mipango iliyosanifiwa, inayowalenga na iliyotahminiwa kwa kuzinagtia taarifa za kina zinazokusanya kutoka mashinani.

Makubaliano hayo yanatoa njia ya mashirika hayo kwa pamoja kutumia taarifa hizo muhimu ili kufanya uratibu ipasavyo kwa lengo la kuhakikisha usaidizi unaohitajika unawafikia watu wanaostahili.

“Makubaliano haya ni hatua muhimu katika juhudi zetu za kuboresha usalama wa chakula nchini Somalia na kutoa njia kutoka kwa usaidizi wa kibinadamu kuelekea uthabiti wa kiuchumi,” alisema mwakilishi wa FAO nchini Somalia, Etienne Peterschmitt.

“Kwa kushirikishana taarifa, tunaweza tukatumia vyema rasilimali zetu na kupiga hatua haraka kuzisaidia jamii zinazokabiliwa na janga.”

Kwa upande wake, Mwakilishi wa WFP na Mkurugenzi wa shirika hilo nchini Somalia El-Khidir Daloum alisema kama mashirika ya kutoa misaada, wamejitolea kuzingatia kanuni za uwazi na uwajibikaji kwa watu wanaowahudumia.

“Utoaji usaidizi kwa njia ya kidijitali na ushirikishanaji wa taarifa utasaidia WFP na FAO kutekeleza mipango ya kuokoa maisha kwa njia madhubuti yanapozihudumia jamii kote nchini Somalia,” aliongeza Daloum.

FAO na WFP ni mashirika mawili makubwa zaidi ya kutoa misaada nchini Somalia, yakitoa usaidizi kwa mamilioni ya watu kila mwezi.

Mashirika hayo hufanya kazi kuwakinga watu wasiojiweza dhidi ya njaa, kuongeza uthabiti wa jamii dhidi ya majanga na kuwawezesha watu na taasisi nchini Somalia kuendeleza mifumo endelevu ya chakula inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Share This Article