Familia yataka haki kufuatia kifo cha binti yao huko Ngong

Marion Bosire
1 Min Read

Familia moja katika kaunti ya Kajiado inataka haki kuhusiana na kifo cha binti yao aliyeaga dunia baada ya kuanguka kutoka kwenye gorofa mjini Ngong.

Daisy Nyakeru Waweru wa umri wa miaka 24 anaripotiwa kuanguka kutoka kwenye orofa ya nne ya jengo moja mjini Ngong kaunti ya kajiado Julai 31, 2024.

Kulingana na ripoti ya polisi, Daisy aliruka mwenyewe lakini familia yake inaamini kwamba alisukumwa na mtu akaanguka akafa.

Washukiwa wanne walikamatwa na polisi kuhusiana na kisa hicho na kati yao ni mwanajeshi mmoja anayefanya kazi katika kituo cha wanajeshi cha Lang’ata ambaye aliachiliwa baadaye.

Mlinzi wa jengo husika alisema alijuzwa kupitia simu kuhusu tukio hilo na alipofika akapata mwili ambao baadaye ulichukuliwa na maafisa wa polisi waliokamata washukiwa pia.

Akizungumza wakati wa mazishi ya Daisy katika makaburi ya Lang’ata Ijumaa Agosti 9, 2024 mamake kwa jina Susan Njeri Mungai alisema anachokitaka ni haki kwa mwanawe hata ingawa ameshamzika.

Wakati alikumbana na mauti, Daisy alikuwa na watu wanne wanawake wawili na wanaume wawili ambao ni washukiwa wakuu wa kifo chake.

Share This Article