Everton inapania kuandikisha ushindi ili kujiondoa katika eneo hatari ya kushushwa daraja itakapowaalika Crystal Palace uwanjani Goodison Park Jumatatu usiku.
Kikosi cha kocha Sean Dyche kinakalia nafasi ya 18 kwenye jedwali la EPL kwa alama 19 baada ya kucheza mechi 24.
Palace kwa upande wao hawako pazuri wakiwa alama tano pekee kutoka eneo la kushushwa ngazo kwa pointi 24 kutokana na mechi 24.
Wenyeji Everton hawajasajili ushindi katika mechi nne zilizopita, wakitoka sare mbili na kupoteza mbili.
Kwenye mechi ya mwisho, Manchester City waliwafunga 2 – 0 uwanjani Etihad. Mabao hayo yalifungwa na mshambulizi Erling Haaland. Katika mechi hizo, wamepokea kichapo cha mabao sita huku wakifanikiwa kufunga mawili.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa katika Kombe la FA raundi ya tatu ambapo Everton ilishinda 1 – 0.
Katika mkondo wa kwanza ya ligi ya EPL uwanjani Selhurst Park, Everton ilishinda 3 – 2.
Kwenye mechi tano zilizopita baina ya timu hizi, Everton imeshinda mechi tatu. Mechi mbili zimeambulia sare tasa.
Palace haijawahishinda mechi uwanjani Goodison Park tangu mwaka wa 2014.
Wachezaji wanaotarajiwa kurejea kwenye kikosi cha Everton ni Ben Godfrey, baada ya kupona kutokana na jeraha alilopata wakicheza dhidi ya Chelsea, Abdoulaye Doucoure, Seamus Coleman na Amadou Onana waliopona majeraha.
Hata hivyo, Arnaut Danjuma, Dele Alli na Andre Gomez wangali wanauguza majeraha.
Kwa upande wa Palace, wachezaji watakaokosa mechi hiyo ni:- Cheick Doucoure, Rob Holding, Michael Olise, Jesurun Rak-Sakyi, Marc Guehi, Eberechi Eze na Will Hughes walio na majeraha.