Eric Omondi asema tatizo sio wasanii wa nje bali ni waandaaji wa matamasha

Maoni yake yanafuatia tafrani iliyoshuhudiwa katika tamasha la Furaha City jijini Nairobi ambapo walinzi wa msanii wa Tanzania Diamond Platnumz wanadaiwa kumdhulumu Willy Paul wa Kenya.

Marion Bosire
2 Min Read

Mchekeshaji na mwanaharakati wa Kenya Eric Omondi amesema kwamba tatizo lililoko sio wasanii wa nchi za nje bali ni waandalizi wa matamasha wa Kenya.

Maoni yake yanafuatia tafrani iliyoshuhudiwa katika tamasha la Furaha City jijini Nairobi ambapo walinzi wa msanii wa Tanzania Diamond Platnumz wanadaiwa kumdhulumu Willy Paul wa Kenya.

Inaripotiwa kwamba Willy Paul alilazimisha kuingia jukwaani kutumbuiza kabla ya Diamond huku mashabiki waliohudhuria hafla hiyo pia wakimpendelea.

Hali hiyo ilisababisha Diamond aondoke bila kutumbuiza.

Omondi anadai kwamba waandalizi wa matamasha humu nchini wanawadharau wasanii wa humu nchini huku wakipendelea wasanii kutoka nje.

Alitaja mambo kama vile kuweka maeneo sawia ya kukaliwa na wasanii wanaposubiri kuingia jukwaani pamoja na mazuri yanayofanana ikiwa ni pamoja na vyakula, ulinzi na usafiri.

Mchekeshaji huyo alizungumzia pia hali ya wafawidhi kujaza mbwembwe wanapokaribisha wasanii kutoka nje jukwaani huku wakiwa hafifu kwa wasanii wa Kenya.

Eric amesema kwamba kudhalilishwa kwa wasanii wa Kenya ambao amekuwa akitetea kwa muda ni lazima kukomeshwe na yeye atakuwa macho kuona jinsi matamasha ya kufunga mwaka yataendeshwa.

Ametishia kushawishi wakenya kususia matamasha kama hayo iwapo wasanii wa humu nchini watadharauliwa na waandalizi wa Kenya.

Eric amesisitiza kwamba wasanii wa Tanzania ni kama ndugu zake kwani hata yeye huenda kutumbuiza humo na mapokezi huwa mema na hivyo tatizo sio wao.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *