Mchekeshaji Eric Omondi amekamatwa akiongoza maandamano ya kundi kwa jina “Mama Mboga Revolution” nje ya majengo ya bunge, alasiri ya leo.
Omondi ambaye alikuwa amevaa mavazi yanayofanana na sare za maafisa wa polisi alikuwa anaongoza kundi la watu waliojitambulisha kuwa mama mboga kwenye maandamano hayo ya kupingwa mswada wa fedha wa mwaka 2024.
Waandamanaji walikuwa wamebeba matawi ya mboga aina ya sukuma wiki ambayo walimwaga nje ya majengo ya bunge.
Maafisa wa polisi waliokuwa wakilinda malango ya bunge walimkamata Omondi na kumpeleka kwenye kituo cha polisi cha bunge na waandamanaji wengine wakatawanyika na kuondoka.
Muda mfupi baadaye video ya tukio hilo ilichapishwa kwenye akaunti ya Omondi ya Instagram na ilikuwa na maneno haya, “Hatutakubali hii serikali iue wakenya na mswada wa fedha wa mwaka 2024.”
Aliendelea kusema kwamba wakenya wanateseka na wengine wanakufa kwenye hospitali bila dawa huku wakenya wakitozwa ushuru ambao kulingana naye unatumiwa na viongozi kununua magari makubwa, nyumba na hata kusafiri nje ya nchi.
Omondi sio mgeni kwa maswala ya maandamano nje ya bunge, mwaka jana alitekeleza maandamano kwa siku kadhaa nje ya bunge akitetea wasanii wa fani mbali mbali nchini.