Mchekeshaji na mwanaharakati Eric Omondi ameorodhesha hatua kadhaa ambazo angechukua iwapo angekuwa Rais wa nchi hii.
Kwenye video aliyochapisha, Omondi anaonekana akihojiwa na mwanahabari wa mitandaoni ambapo anasema hatua ya kwanza ambayo angechukua kama Rais ni kupunguza idadi ya kaunti humu nchini.
“Iwapo ningepatiwa mamlaka kama Rais hata kwa siku moja, kitu cha kwanza ambacho naweza kufanya ni kupunguza idadi ya kaunti kutoka 47 hadi 8 pekee.” alisema Omondi.
Alisema pia kwamba angepunguza idadi ya wabunge kutoka zaidi ya 300 hadi 50 pekee, huku akipunguza pia matumizi katika afisi yake.
Omondi anasema ataondoa wadifa wa naibu gavana, aondoe bunge la seneti, aondoe nyadhifa za wabunge wateule na kupunguza idadi ya wawakilishi wodi.
Msanii huyo alisema kwamba pesa atakazookoa kufuatia mabadiliko hayo atawekeza katika elimu bila malipo, huduma bora za matibabu bila malipo na kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa.
Omondi amekuwa mkosoaji mkuu wa utawala wa sasa wa Kenya ambao anahisi hauendeshi nchi kwa njia inayofaa.