Shirikisho la Soka Nchini Equatorial Guinea limewatimua kocha na wachezaji wa timu ya taifa kwa kugoma na kukataa kusafiri kwenda Malawi wiki jana kwa mchuano wa kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Kocha na wachezaji waligoma wakitaka walipwe marupurupu yao.
Equatorial Guinea inakabiliwa na hatari ya kuwekewa vikwazo pamoja na kutozwa faini na FIFA kwa kosa hilo.
Kocha mkuu Juan Micha na wanandinga kadhaa wakiwemo nahodha Emilio Nsue, wametemwa kwenye kikosi kitakachochuana na Liberia katika mchuano wa kundi H, Jumatatu.
Taarifa kutoka kwa Wizara ya Michezo nchini humo imesema imewapa wachezaji chipukizi fursa ya kujitangaza na kulinda hadhi ya nchi.
Casto Nopo ameteuliwa kaimu kocha wa kikosi hicho.