Mamlaka ya kawi nchini EPRA imeagiza kufungwa kwa vituo vyote vya kuuza mafuta vilivyofurika ili kutoa fursa ya kutathminiwa kwa ubora wa mafuta ambayo yamehifadhiwa kwenye tangi za ardhini.
Mkurugenzi mkuu wa EPRA Daniel Kiptoo alisema kupitia taarifa jana kwamba ni muhimu kwa wamiliki wa vituo hivyo kuhakikisha kwamba ubora wa bidhaa zao haujaathiriwa na maji ya mafuriko.
EPRA hata hivyo haikutaja hatua zitakazochukuliwa dhidi ya watakaokiuka agizo hilo la Jumatano Mei Mosi, 2024.
Mafuta yaliyoathirika huwa hatari kwa injini za magari na hatua ya EPRA inaonekana kama hatua ya kulinda wateja dhidi ya hasara ya aina yoyote ambayo huenda wakaingia kwa kulazimika kukarabati injini za magari yao au hata kuzibadilisha.
Wateja kadhaa wa Nairobi tayari wameripoti visa kama hivyo vya kujaziwa mafuta ambayo yameingiwa na maji na uchafu kufuatia mafuriko yanayoshuhudiwa nchini.
Sheria ya kawi ya mwaka 2019 imetoa adhabu ya faini ya shilingi milioni 5 au kifungo gerezani kisichozidi miaka miwili kwa yeyote atakayepatikana akiuza mafuta ambayo ubora wake ni wa kutiliwa shaka.