Elon Musk na Prince Andrew watajwa kwa nyaraka mpya za Epstein

BBC
By
BBC
5 Min Read

Bilionea Elon Musk na Prince Andrew wametajwa katika nyaraka mpya zilizotolewa na wanachama wa chama cha democratic wa bunge la Marekani zinazohusiana na marehemu mfadhili na mkosaji wa kingono aliyekutwa na hatia, Jeffrey Epstein.

Nyaraka hizo, ambazo zilikabidhiwa kwa Kamati ya Usimamizi ya Bunge na Urithi wa Jeffrey Epstein, zinaonekana kuonyesha kuwa Musk aliwahi kualikwa kwenye kisiwa cha Epstein mnamo Desemba 2014.

Kwa upande mwingine, orodha ya abiria ya ndege kutoka New Jersey hadi Florida mwezi Mei 2000 inamtaja Prince Andrew miongoni mwa abiria.

Prince Andrew hapo awali amekanusha vikali kufanya kosa lolote. Musk pia alinukuliwa akisema kuwa Epstein alimwalika kisiwani lakini alikataa mwaliko huo.

Nyaraka hizi za awali ni sehemu ya kundi la tatu la hati zilizotolewa na Urithi wa Epstein.

Wademokrat katika Kamati ya Usimamizi ya Bunge wanasema nyaraka hizo zinajumuisha rekodi za ujumbe wa simu, nakala za orodha za safari za ndege, nakala za vitabu vya fedha na ratiba ya kila siku ya Epstein.

Mbali na Musk na Prince Andrew, nyaraka hizo pia zinataja majina ya watu mashuhuri wengine wakiwemo mjasiriamali wa mtandao Peter Thiel na Steve Bannon, mshauri wa zamani wa Donald Trump.

Mstari mmoja kwenye nyaraka ulioandikwa tarehe 6 Desemba 2014 unasomeka: “Kumbusho: Elon Musk kwenye kisiwa Dec. 6 (je, hii bado ipo?)”

Orodha ya safari ya ndege inaonyesha kuwa Prince Andrew alikuwa kwenye ndege pamoja na Epstein na mshirika wake Ghislaine Maxwell kutoka Teterboro, New Jersey hadi West Palm Beach, Florida, tarehe 12 Mei 2000.

Maxwell alihukumiwa mwaka 2021 kwa kula njama na Epstein kuwateka wasichana kwa ajili ya ngono.

Kitabu kimoja cha fedha, ambacho kimehaririwa sana, kinarekodi malipo mawili kwa ajili ya “masaji” kwa mtu anayeitwa Andrew mwezi Februari na Mei 2000.

Ingawa kumbukumbu za kasri, picha na ripoti za vyombo vya habari wakati huo zinaonyesha kuwa Prince Andrew alisafiri kwenda Marekani karibu na tarehe hizo, haijathibitishwa wazi iwapo “Andrew” aliye katika rekodi hiyo ni Prince Andrew.

Mnamo tarehe 11 Mei 2000, Kasri la Buckingham lilisema kupitia tovuti yake kwamba Prince Andrew alisafiri kwenda New York kuhudhuria hafla ya shirika la National Society for the Prevention of Cruelty to Children. Aliyarudi Uingereza tarehe 15 Mei, kwa mujibu wa taarifa nyingine ya kasri hilo.

Prince Andrew amekanusha mara kadhaa kufanya makosa yoyote katika urafiki wake na Epstein.

Katika nyaraka hizo pia kuna kumbukumbu ya chakula cha mchana kilichopangwa na Peter Thiel mnamo Novemba 2017.

Kuna pia kumbukumbu ya kifungua kinywa kilichopangwa na Steve Bannon tarehe 17 Februari 2019.

Nyaraka hizo pia zinataja mipango ya awali ya hafla ya kifungua kinywa pamoja na mwanzilishi wa Microsoft, Bill Gates, mwezi Desemba 2014.

Mwaka 2022, Gates aliiambia BBC kuwa kukutana na Jeffrey Epstein kulikuwa “kosa”.

Hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa watu waliotajwa kwenye nyaraka hizo walikuwa wanajua kuhusu shughuli za uhalifu ambazo Epstein alishtakiwa nazo baadaye.

Epstein alifariki kwa kujiua katika seli ya gereza mjini New York mnamo Agosti 2019 akiwa anasubiri kesi ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono.

Mnamo 2008, alifikia makubaliano na waendesha mashtaka baada ya wazazi wa msichana wa miaka 14 kuripoti kwa polisi kwamba Epstein alimdhalilisha binti yao nyumbani kwake Palm Beach. Alikamatwa tena mwezi Julai 2019 kwa mashitaka ya usafirishaji wa watu kwa ajili ya ngono.

Sara Guerrero, msemaji wa Wademokrat katika kamati hiyo, alimtaka Mwanasheria Mkuu Pam Bondi kutoa nyaraka zaidi zinazohusiana na Epstein.

“Inapaswa kuwa wazi kwa kila Mmarekani kuwa Jeffrey Epstein alikuwa na urafiki na baadhi ya watu wenye nguvu na utajiri mkubwa duniani. Kila hati mpya inayoletwa inatoa taarifa mpya tunapojitahidi kuleta haki kwa waathiriwa,” alisema.

Warepublikan katika kamati hiyo waliwalaumu Wademokrat kwa “kutoa siasa kuliko kutetea waathiriwa” na walisema wataachilia seti kamili ya nyaraka hivi karibuni.

BBC
+ posts
Share This Article